Jumanne 16 Juni 2026 - 21:00
Lengo la Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ni kuitumikia jamii kwa ikhlasi

Hawza/ Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, amesisitiza kwamba; shughuli za vitengo mbalimbali vya harakati hiyo kwa hakika zinafanyika kwa ajili ya “kuokoa na kuitumikia jamii.”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Zakzaky aliyasema hayo katika hafla ya kufunga Kongamano la Ishirini na Nane la “Jumuiya ya Tiba ya Kiislamu” (ISMA), lililofanyika katika makazi yake mjini Abuja.

Akirejelea shughuli za Jumuiya ya Tiba ya Kiislamu, alizielezea juhudi hizo kuwa ni muhimu sana na zenye lengo la kuokoa maisha ya watu, na akaongeza kuwa; huduma za tiba na kijamii zinazotolewa na taasisi hiyo zina mchango mkubwa katika kuwasaidia wananchi.

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pia alizungumzia shughuli za kamati nyingine na vitengo mbalimbali vya harakati hiyo katika nyanja tofauti za kijamii na kusema: “Hatua zote hizi kwa hakika zinafuatilia lengo moja la pamoja, nalo ni kushughulikia masuala ya jamii na kuwahudumia watu.”

Sheikh Zakzaky alisisitiza kwamba; shughuli hizi ni ushahidi wa nia njema na mtazamo chanya wa harakati hiyo kwa jamii; jambo ambalo, kwa mujibu wake, ni kinyume na taswira ambayo wapinzani wanajaribu kuionesha kuhusu harakati hiyo.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alionesha wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kulevya na madhara yake katika jamii, na akaonya kwamba; maadui wanatumia dawa za kulevya kama nyenzo ya kuharibu malezi ya vijana na kuwapeleka katika tabia potovu.

Mwishoni mwa hotuba yake, Sheikh Zakzaky alitoa wito wa kuendelezwa shughuli za huduma na kazi za kijamii kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, na akasisitiza umuhimu wa kuunga mkono mipango kama hiyo, akisema: “Kuihudumia jamii inapaswa kuendelea kwa ikhlasi na kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha